Sunday, October 13, 2019

Jamii Yaaswa Kushiriki Kuzuia na Kupunguza Athari za Maafa

Na Mwandishi Wetu
Jamii imeaswa kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kupunguza athari za maafa pale yanapotokea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
 
Aklizunmgumza leo Oktoba 13, 2019 Jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Upunguzaji wa Athari za Maafa Duniani ambapo alikuwa mgeni rasmi, Katibu mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko amesema suala hilo linahitaji ushirikiano wa jamii nzima.
 
“Tumekutana leo hapa tukishirikiana na wenzetu Duniani kote kukumbushana mbinu na mikakati ya kupambana na maafa ikiwemo kuweka mikakati ya kupunguza maafa yanapotokea katika maeneo yetu”Alisisistiza Bi Mwaluko
 
Akifafanua amesema kuwa, Wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) wanaosomea Shahada ya udhibiti wa maafa katika mazingira washiriki kikamilifu katika kutoa elimu kuhusu maafa katika shule za Sekondari na msingi zilizopo hapa Dodoma  kupitia chama cha udhibiti wa maafa katika chuo hicho.
 
Aliongeza kuwa wanafunzi hao wanatakiwa kuwa chachu katika kutoa elimu kuhusu maafa ili kupanua wigo wa elimu na kuagiza chama hicho kuhakikisha kuwa kinawasilisha mpango wake wa utoaji elimu katika Ofisi yake.
 
Aidha, Bi Mwaluko ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha ili waweze kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuchagua viongozi watakaosaidia katika kuleta maendeleo kwa kusimamia kikamilifu rasilimali zinazotolewa na Serikali kwa maslahi ya wananchi.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri mkuu, Kanali Jimmy Said amesema kuwa Sera ya Maafa inaelekeza kikamilifu majukumu ya kamati za maafa katika ngazi zote ili kurahisisha mawasiliano na kuimarisha utendaji .
 
Aliongeza kuwa kila mwananchi anapaswa kutimiza wajibu wake katika eneo lake ili kupunguza athari za maafa pale yanapotokea.
 
Siku ya maafa huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 13, ya kila mwaka ili kuwaleta pamoja wadau kujadili na kuweka mikakati ya pamoja katika kupambana na maafa.




from MPEKUZI https://ift.tt/2pdrWXF
via IFTTT

No comments:

Post a Comment