Wednesday, October 2, 2019

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Laua Majambazi Watatu

Jeshi  la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limewaua watuhumiwa wa ujambazi watatu akiwamo aliyeuawa nje ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, alisema jana kuwa katika tukio la kwanza, Jeshi la Polisi limemuua mtuhumiwa Emmanuel Peter ambaye alikuwa anasakwa kwa muda mrefu.

Alisema mauaji hayo yalitokea juzi eneo la Ilala Boma majira ya mchana, ambapo polisi ilipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa mtuhumiwa huyo yupo na wenzake wanne.

Kamanda Mambosasa alisema kikosi kazi kilifika eneo hilo la tukio na kumkuta mtuhumiwa huyo na ghafla alishtukia amezungukwa na askari, ndipo alipotoa silaha kwa nia ya kuwafyatua risasi polisi.

“Polisi waliokuwa eneo la tukio walimuwahi na kumjeruhi mtuhumiwa huyo na kumnyang’anya bastola ikiwa na risasi mbili, risasi moja ikiwa chemba imepakiwa tayari kwa kufyatuliwa,” alisema.

Alisema mtuhumiwa huyo alipelekwa hospitali, lakini alifariki dunia na mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Katika tukio la pili, Mambosasa alisema Alhamisi iliyopita mchana eneo la Mbezi Msakuzi njia panda ya Mpiji Magoe.

“Tulipata taarifa kuna watuhumiwa wa ujambazi ambao wamejipanga kwenda kuvamia Vyama vya Akiba na Mikopo (Saccos) ya Msakuzi. Tuliweka mtego na ilipofika saa sita mchana zilifika pikipiki mbili aina ya Boxer ambazo hazikusomeka namba zake zikiwa na watu wanne, mmoja akiwa na bastola,” alisema.

Alisema watu hao walipogundua wanafuatiliwa, walikimbia ndipo askari walipofyatua risasi kwa nia ya kuwasimamisha, lakini nao walijibu mapigo.

Alisema katika majibizano ya risasi, polisi iliwajeruhi watuhumiwa wawili ambao walifariki dunia baadaye na wengine walikimbia.

Alisema majeruhi hao walikutwa na bastola moja na risasi tatu ndani ya magazine na maganda mawili ya risasi.


from MPEKUZI https://ift.tt/2pa60fL
via IFTTT

No comments:

Post a Comment