Monday, October 14, 2019

JPM Anamuenzi Nyerere Kwa Vitendo-RC Mtaka

Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema serikali ya awamu ya tano chini ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe inamuenzi Hayati Baba wa Taifa, Mwl Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo hususani katika kuendeleza kazi nzuri alizozifanya.

Mtaka ameyasema hayo Oktoba 14, 2019 katika Kongamano la Kitaifa la Kumbukizi ya Miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere lililofanyika Oktoba 14, 2019 Mjini Bariadi, likiwashirikisha viongozi wa Serikali, wananchi na baadhi ya viongozi wa CCM Mkoa wa Simiyu, UVCCM Simiyu, UVCCM kutoka mikoa mbalimbali nchini na ngazi ya Taifa(makao makuu).

“Mwalimu amepewa heshima ya kuenziwa ninyi  kizazi hiki mnashuhudia kwa macho, wapo watu wanasimuliwa tu kuwa ile barabara inaitwa ‘Nyerere road’, lakini hamkuwepo; leo mnajua kwamba hifadhi fulani inaitwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, mnasikia Mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa  J.K. Nyerere,  Mhe.Rais amemheshimisha Mwalimu kwa vitendo,” alisema Mtaka

“Mwalimu aliamini katika Watanzania kufanya shughuli za kiuchumi  ikiwemo kilimo,  ufugaji na uvuvi  na akataka waongeze thamani katika shughuli hizo; ndiyo maana Mhe Rais ameanza kufufua viwanda vya nguo, viwanda vya korosho, viwanda vya kahawa na mengine aliyoyaacha Mwalimu, “ aliongeza Mtaka.

Aidha, Mtaka amemzungumzia Mwalimu Nyerere kuwa alikuwa kiongozi wa karne mwenye utu, maono na msimamo ambaye alijua wapi anapotoka na anapotakiwa kwenda kama kiongozi na aliyewaheshimisha Watanzania.

Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa Vijana wa UVCCM  kuwaeleza ukweli na kuwashauri viongozi vijana ndani ya Serikali kufanya kazi zao kwa kuzingatia misingi ya uongozi na kuepukana na tabia ya kuweka urasimu wa kufikika na watu , ili viongozi hao watekeleze vema wajibu wao wa kuwatumikia wananchi na kumsaidia Mhe. Rais Magufuli katika majukumu aliyowapa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe.Enock Yakobo amewataka vijana kumuenzi Hayati  Baba wa Taifa, Mwl. Julius K. Nyerere kwa kufanya kazi kwa bidii, ili wajiletee maendeleo kwa kuwa Mwalimu aliamini kuwa kazi ni kipimo cha uhai.

Naye Kaimu Katibu Idara ya Mahusiano ya Kimataifa na Vyuo Vikuu, Bi Asha Feruz amesema kwa kuwa vijana wengi wamezaliwa wakati Hayati Baba wa Taifa,Mwl. Julius K. Nyerere akiwa amefariki ni vema vijana hao wakasoma  vitabu, ili wajue historia ya mwalimu na waasisi wengine wa Taifa la Tanzania.

Mmoja wa Wajukuu wa Mwalimu Nyerere Chifu Edward Magige amesema pamoja na Watanzania kuendelea kukumbuka na kuenzi mambo mazuri yaliyofanywa na Hayati Mwalimu Nyerere ni vema pia wakaukumbuka mchango wa Mama Maria Nyerere katika kazi zilizofanywa na mwalimu.

Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe. Njalu Silanga ametoa wito kwa Vijana hapa nchini kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura, ili waweze kuitumia vema haki yao kuchagua viongozi bora ikiwa ni namna mojawapo ya kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuchagua viongozi watakaosimamia misingi ya uongozi aliyoiweka.

MWISHO


from MPEKUZI https://ift.tt/2MeDPFy
via IFTTT

No comments:

Post a Comment