Thursday, October 17, 2019

Mifuko Ya Uwezeshaji Kiuchumi Yatakiwa Kuwawezesha Wananchi Mitaji Waanzishe Viwanda

Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga ametoa wito kwa Mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kuangalia jinsi ya kuwezesha wananchi wengi zaidi kupata mitaji ya kuanzisha viwanda, ili uchumi wa nchi ukue na kupunguza changamoto zinazokabili jamii.

Kiswaga ameyasema wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika uzinduzi wa Maonesho ya tatu ya  mifuko/programu za uwezeshaji na vikundi vya kifedha  vya kijamii, uliofanyika Oktoba 16, 2019  katika Uwanja wa Halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

“Sote tunafahamu kwamba Tanzania inalenga kufikia uchumi wa katika ifikapo mwaka 2025 na viwanda ni nyenzo itakayowezesha nchi kufika huko; viwanda vina mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi  kwa kuwa vinanufaisha jamii kwa kutoa ajira, kulipa kodi, kununua malighafi kutoka kwa wakulima na mengine mengi,” alisema Kiswaga.

Aidha, Kiswaga alitoa wito kwa wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa na maeneo mbalimbali nchini kufika katika maonesho haya kupata maelezo kutoka kwa wawakilishi wa mifuko /programu za uwezeshaji za Serikali, kuonesha bidhaa, kunua bidhaa za wajasiriamali na kupata uelewa wa masuala ya uwezeshaji wananchi.

Naye Afisa Maendeleo ya Biashara wa Taasisi ya kusaidia sekta binafsi na Kilimo,  (PASS) Kanda ya Ziwa, Faustine Mungo amesema wameandaa mpango mkakati wa miaka mitano ambapo wanatarajia kutoa ajira 700,000 ambao unatarajia kuzifikia familia zaidi ya 200,000.

Kaimu Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Ushiriki wa Watanzania katika Uwekezaji, Bi.Esther Mmbaga kutoka Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi(NEEC), amesema malengo ya maonesho haya ni pamoja na kukuza uelewa wa wananchi  kuhusu uwepo, majukumu na vigezo katika kutoa huduma za mikopo na programu za uwezeshaji.

Bi. Mmbaga ameongeza kuwa malengo mengine ni kuhamasisha wananchi ili waweze kunufaika na fursa zilizopo katika mifuko na programu za uwezeshaji na kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza katika miradi yenye tija.

Maonesho ya tatu ya  mifuko/programu za uwezeshaji na vikundi vya kifedha  vya kijamii, yenye Kauli Mbiu “Mitaji ni Chachu ya Kujenga Uchumi wa Viwanda”ambayo yanaendelea katika uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi yanatarajiwa kufungwa rasmi Oktoba 20, 2019 .

MWISHO


from MPEKUZI https://ift.tt/31k6IEB
via IFTTT

No comments:

Post a Comment