Tuesday, October 1, 2019

Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam Yakamata Magari 50 huku 19 Yakiwa ya Serikali Kwa Kosa la kupita katika barabara ya mabasi ya mwendokasi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa, amesema Jeshi la polisi kwa kipindi cha kuanzia Septemba 19, 2019 hadi sasa linashikilia jumla ya magari 50 huku 19 yakiwa ya Serikali na 31 binafsi kwa kosa la kupita katika barabara ya mabasi ya mwendokasi.

Akizungumza leo Oktoba 1, 2019 Kamanda Mambosasa amesema kuwa japo kuna watu wamezoea kutoa faini pindi wanapokiuka sheria, lakini kwa upande wa barabara ya mwendokasi hakutakuwa na utaratibu wa kutoza faini badala yake watu watapelekwa rumande.

''Unakuta mtu anandaa fedha kwanza afu anaingia mwendokasi kwakuwa faini ni elfu 30, katika mwendokasi sitakubali kutoza faini, hatuko kwa ajili ya kutafuta fedha tunachotaka nikuleta nidhamu ya matumizi sahihi ya barabara hiyo, atakamatwa mhusikia atapelekwa polisi, atawekwa rumande maandalizi yatafanyika kupelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali na kufunguliwa mashtaka'' amesema SACP Mambosasa.

Kamanda Mambosasa ameongeza kuwa magari pekee yanayoruhusiwa kutumia njia hizo ni yale yanayowahisha wagonjwa hospitali na kwamba ikitokea gari la wagonjwa limetumia njia hiyo likiwa halina mgonjwa lazima litakamatwa.


from MPEKUZI https://ift.tt/2mAgioA
via IFTTT

No comments:

Post a Comment