Thursday, October 10, 2019

Taasisi Za Umma Zapigwa Marufuku Kutumia Kampuni Binafsi Katika Masuala Ya Tehama

Na James K. Mwanamyoto, Namtumbo
Serikali imepiga marufuku taasisi za umma nchini kutumia fedha za Serikali kuilipa taasisi binafsi ili kupatiwa huduma ambazo pia zinazotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) ametoa agizo hilo kwa watumishi wa umma na waajiri Serikalini, wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, Serikali imebadili Wakala ya Serikali Mtandao kuwa Mamlaka kwa sababu hivi sasa ina wataalamu wa kutosha wa TEHAMA hivyo hakuna ulazima wa kuilipa kampuni binafsi ili kupata huduma ya TEHAMA.

“Kama Serikali ina chombo chenye uwezo na weledi wa kutosha wa kutoa huduma za TEHAMA ikiwemo mifumo ya kielektroniki ya utoaji huduma, ni nini kinachoshinikiza Taasisi za Umma kuendelea kuomba kupatiwa huduma hiyo na kampuni za watu binafsi?,” Mhe. Mkuchika amehoji.

Mhe. Mkuchika yuko katika ziara ya kikazi mkoani Ruvuma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo.


from MPEKUZI https://ift.tt/2nDuqy4
via IFTTT

No comments:

Post a Comment