Sunday, October 6, 2019

Takukuru Ichunguze Watumishi 48 Iramba Kwa Upotevu Wa Fedha ....Asema Ikithibitika Ni Kweli, Lazima Warudishe Fedha Hizo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Bw. Adili Elinipenda achunguze watumishi 48 waliojihusisha na upotevu wa fedha kwa njia za udanganyifu.

Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumapili, Oktoba 6, 2019), wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmshauri hiyo.

Waziri Mkuu ametoa maeneo saba ambayo ametaka yafanyiwe uchunguzi wa kina ili kubaini upotevu huo. Eneo la kwanza ni upotevu wa makusanyo ya ndani kupitia mawakala wa ukusanyaji mapato (POS) ambapo mawakala wanaokusanya fedha wanashirikiana na watumishi wa Halmashauri na kuzitumia bila kuziingiza benki.

Kuna kundi la watumishi 10 wakiongozwa na mtu wa TEHAMA, wameshirikiana kupata password na fedha zikishakusanywa wanazitoa na kuzitumia bila kuzipelekea benki. Wamesahau kwamba malipo yalipoingizwa mara ya kwanza, data ilirekodiwa kwenye mfumo wa malipo na sisi tunaona ni kiasi gani kimekusanywa.”

Watumishi hao ni Salum Omari (Mtaalamu wa TEHAMA); Adam Mzengi (Mhasibu kahamishiwa Gairo); Rafaeli Nasari; Caroline Makundi (kahamishiwa Singida Manispaa), Edson S. Ally (Afisa Biashara); Martin Kimisho (Mhasibu Msaidizi); Prosper Banzi (Afisa Biashara); Hassan Ponda (Mhasibu kituo cha afya Ndago); Hafidh Ngayunda (Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya) na Muhidin Mohammed (Mweka Hazina wa Wilaya) ambaye tayari amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma hizo.

Kutokana na upotevu huo, Waziri Mkuu ameagiza Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya akae pembeni hadi uchunguzi wa TAKUKURU utakapokamilika.

Akibainisha mchezo mwingine uliochezwa na watumishi wa Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu amesema kuna watumishi 38 ambao walilipwa kiasi cha sh milioni 46 ambazo zilikuwa sehemu ya sh. milioni 400 za kujenga vituo vya afya vya Ndago na Kinampanda wilayani humo.

“Hapa nina vocha zote za malipo walipeana fedha watu hawa akiwemo Mkurugenzi wao. Lakini ni kazi gani ambayo kundi lote hili lilikuwa likiisimamia na kustahili kupata malipo hayo? Kutoka makao makuu ya wilaya hadi Ndago au Kinampanda kuna umbali gani?” alihoji Waziri Mkuu.

“Kamanda wa TAKUKURU fanya uchunguzi, fuatilia wote waliohusika sababu majina tunayo, kama hawastahili kulipwa ni lazima warudishe fedha yetu. Hii ni sehemu ya sh. milioni 90 ambazo hazijulikani ziliko na zilikuja kujenga kituo cha afya. Fedha hizi zimekuja na maelekezo rasmi, ni kwa nini zilibadilishwa matumizi,” alihoji.

Waziri Mkuu alisema kuna fedha ya walimu sh. milioni 29 ambayo ilitumwa na TAMISEMI ili kulipa likizo zao lakini Mkurugenzi alitumia kulipia usafirishaji wa makontena ya vifaa vya tiba kutoka Sweden hadi Singida wakati mkataba wa malipo unasema Halmashauri ilipaswa kulipia kutoka bandari ya Tanga hadi Singida.

“Hii fedha ya walimu ya likizo nataka irudishwe mara moja. Pia kuna shilingi milioni 6.86 ambazo mmedai ni malipo ya kukomboa mizigo bandarini wakati vifaa hivyo vilipata msamaha wa kodi. Tena kuna sh. milioni 34 ambazo zililetwa kurekebisha Ikama za walimu lakini hadi leo hazijalipwa. “Kamanda wa TAKUKURU nataka uniambie nafasi ya Afisa Elimu ikoje kwenye suala hili,” alisema.

Pia alisema kuna fedha kujenga machinjio ya kisasa ambayo ililetwa lakini machinjio hayajakamilika hadi sasa. “Tumeleta sh. milioni 100 za machinjio lakini Afisa Mifugo anasema wametumi sh. milioni 20 tu, nataka sh. milioni 80 zimeenda wapi.”

Waziri Mkuu alisema kuna sh. 18,090,000 za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kutoka vituo vya afya 13 ambazo zimetumika kusafirisha hayo makontena nayo pia irudishwe. “Hivi mnachangisha watu sh. 30,000 kwa ajili ya kupata dawa wakienda kutibiwa lakini leo hawana dawa kwa sababu mmezitumia ndivyo sivyo na wao hawana dawa kwenye vituo hivyo kwa sababu hamjazirejesha.”

“Kamanda wa TAKUKURU fanya uchunguzi kwenye fedha ya mikopo ya akinamama, vijana na wenye ulemavu ambayo ni asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri. Fedha hii haijatoka tangu mwaka 2017/2018 na 2018/2019.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI https://ift.tt/2IrLSMS
via IFTTT

No comments:

Post a Comment