Wednesday, October 9, 2019

TAKUKURU Yaieleza Mahakama Ilivyomnasa Mhadhiri Akiomba Rushwa ya Ngono Kwa Mwanafunzi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeelezwa kuwa, maafisa wa Takukuru walimkuta Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samson Mahimbo (68) akijiandaa kufanya ngono na mwanafunzi wake.
 

Hayo yameelezwa jana Jumatano Oktoba 9, 2019 na wakili wa taasisi hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania,  Faraja Salamba wakati akimsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi. 

Salamba amedai wakati wa tukio hilo mhadhiri huyo alikuwa mwajiriwa wa NIT akifundisha wanafunzi wa muhula wa kwanza wa masomo wa mwaka  2015/2016 somo la usimamizi wa barabara na usafirishaji.

Amedai Januari 5 na 11, 2017 mshtakiwa alitumia madaraka yake vibaya kwa kuomba rushwa ya ngono na alimpigia simu Victoria na kumsisitiza wakutane katika baa ya Shaniiliyopo maeneo ya Mwenge.

Walipokutana , mshitakiwa alikuwa na mtihani wa marudio ambao Victoria alitakiwa kufanya, karatasi ya majibu na marking scheme ambapo alimsahihishia na kumpa alama 67 na baada ya kumaliza wakuhamia kwenye baa na nyumba ya kulala wageni inayoitwa Camp David , iliyopo Mlalakuwa Mwenge.

Amedai wakiwa pale walikunywa na kulewa kisha wakachukua chumba na kuingia ndani na kwamba mshitakiwa alianza kuvua nguo na kubaki na nguo ya ndani.

"Mshitakiwa alianza kumkumbatia Victoria na kuanza kumvua nguo zake na mara walisikia mlango ukigongwa na Victoria aliufungua na kuingia maofisa wa Takukuru, muhudumu wa baa na mjumbe. Walikuta nguo zipo juu ya meza," alidai.

Mshtakiwa alikamatwa na Januari 12, 2017 alienda kuandika maelezo Takukuru na Agosti 14, mwaka huu aliletwa mahakamani.Mshitakiwa alikana maelezo hayo na kukubali majina yake na mahali anapokaa.

Upande wa mashitaka ulidai kuwa wanamashahidi sita na vielelezo saba ili kuthibitisha mashitaka hayo huku mshitakiwa huyo alidai atakuwa na mashahidi wanne.

Maimu alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na mashitaka ya kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa chuo hicho.


Mhadhiri huyo anadaiwa akiwa mwajiriwa wa NIT alikuwa akifundisha wanafunzi wa muhula wa kwanza wa masomo wa mwaka 2015/16.

Anadaiwa alitenda kosa hilo Januari 12, mwaka 2017 katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Camp David

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo akiwa mwajiriwa wa NIT katika kozi ya Usimamizi wa Barabara na Usafirishaji namba LTU 07101 alitumia mamlaka yake alimlazimisha mwanafunzi huyo kutoa rushwa ya ngono.

Ilidaiwa kuwa, aliomba rushwa hiyo ili aweze kumfaulisha katika mtihani wake wa marudio katika kozi ya Usimamizi wa Barabara na Usafirishaji uliokuwa unafanyika Januari 5 ,mwaka 2017.

Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana na keshi itaanza kusikilizwa Novemba 11, mwaka huu.


from MPEKUZI https://ift.tt/2VAMk0Y
via IFTTT

No comments:

Post a Comment