Friday, December 6, 2019

Serikali Za Mitaa Zatakiwa Kuwa Na Mpango Mkakati Katika Uzoaji Taka

Taasisi zote za Umma na Serikali za Mitaa zimetakiwa  kuwa na Mpango Mkakati wa kisera, kikanuni na kimuundo katika uzoaji taka nchini na kuhakikisha kwamba taka zote zinatolewa ama kurejelezwa kuwa malighafi ya kutengeneza vitu vingine. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mh George Simbachawene alipokua akifungua mdahalo wa udhibiti wa taka Nchini. Ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaama katika Ukumbi Nkurumah.

Akiongea katika mdahalo huo aliongeza kuwa Tafiti mbalimbali zinaonyesha wananchi wana utayari mkubwa katika kuchangia huduma za uzoaji Taka. 

Kwa Mfano, katika tafiti iliyofanywa 2019 chini mradi wa Institutional for Inclusive Development umeonesha mji wa Arusha zaidi ya asilimia 90 ya wananchi huchangia gharama za huduma ya taka, wakati Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ni kati ya asilimia 70-80, mji wa Dodoma ni asilimia 70, na Ilala asilimia 70 ya wananchi huchangia huduma husika.

“Udhibiti wa taka ngumu ni muhimu sana katika utunzaji wa mazingira na afya za viumbe hai kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho. Sheria ya usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 Kifungu cha 114-119, vinazungumzia masuala ya udhibiti wa taka ngumu.” Alisema Waziri Simbachawene

Aidha aliongeza kuwa Kumekuwa na jitihada mbalimbali ambazo Serikali Kuu pamoja na Halmashauri za Miji na Majiji kupitia Serikali za Mitaa zimetekelezwa. Jitihada hizi ni pamoja na: Kampeni mbalimbali katika kuhakikisha hali ya udhibiti wa taka ngumu inamarika. 

Miongoni kwa kampeni hizo ni kama vile Ushirikishwaji wa jamii kufanya usafi kila jumamosi; Ubinafsishaji wa shughuli za uzoaji taka kwa kutumia kampuni binafsi na vikundi vya kijamii (CBOs); Uanzishwaji wa kanuni za udhibiti wa Taka ngumu za mwaka 2009 (Environmental (Solid Waste Management) Regulations, 2009) chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 na Uanzishwaji wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za kupiga marufuku mifuko ya plastiki za Mwaka 2019.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaama Profesa Donata Tibuhwa akimkaribisha Mgeni Rasmi alisema kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaama kimeaandaa mdahalo huo juu ya udhibiti wa taka na kuupa jina la ‘TANZANIA BILA TAKA” na wamefanya hivyo kuunga mkono jitihada za Serikali juu ya utunzaji wa mazingira. Alisema kuwa wanaipongeza Serikali ya awamu ya tano kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kufanikisha upigaji marufuku wa mifuko ya plastiki ( kwani mifuko ya plastiki ni hatari kwa afya).

Mdahalo huo umeandaliwa na Chuo kikuu cha Dar es Salaama na kuwezesha mada mbalimbali kutolewa na kujadiliwa kwa kina. Mdahalo huo ulifanyika katika Ukumbi wa Nkuruma na ulishirikisha Wanafunzi pamoja na Wadau mbalimbali wa masuala ya mazingira ikiwemo usimamizi wa taka.



from MPEKUZI https://ift.tt/2YoMDxc
via IFTTT

No comments:

Post a Comment