Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeshinda tuzo mbili ikiwemo mshindi wa jumla katika uandaaji bora wa taarifa za hesabu mwaka 2018 kwa kufuata viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu katika Taasisi za Umma yaani mfumo wa IPSASs.
Katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha NBAA Bunju jijini Dar es Salaam, TRA imeibuka mshindi wa kwanza katika uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwenye kipengele cha Wakala wa Serikali na mshindi wa jumla kwa taasisi, wakala, kampuni na mashirika mbalimbali ambayo yamefanya vizuri katika kuandaa taarifa za fedha katika shughuli zao za kila siku.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Kamishna Mkuu wa TRA Dkt. Edwin Mhede, ameipongeza Idara ya Fedha na idara nyingine ndani ya mamlaka hiyo kwa kufanikisha upatikanaji wa tuzo hizo.
“Nachukua nafasi hii kumshukuru mkuu wa idara anayehusika na Idara ya Fedha pamoja na wakuu wa idara nyingine ndani ya mamlaka maana zote zinatoa mchango mkubwa kuhakikisha idara hii inatoa taarifa sahihi na zenye kuleta mipango sahihi kwa mamlaka na serikali kwa ujumla,” alisema Dkt. Mhede.
Dkt. Mhede alieleza kuwa, taarifa sahihi ni msingi wa mipango kwa kuwa taasisi isiyopanga kushinda ni sawa na taasisi inayopanga kushindwa hivyo suala la uandaaji bora wa taarifa za hesabu ni moja ya ufanisi wa ofisi yoyote hapa ulimwenguni.
Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) ndio hutoa tuzo hizo kila mwaka ambapo mwaka 2017 TRA iliibuka mshindi wa kwanza tena katika uandaaji bora wa taarifa za hesabu katika kipengele cha Wakala wa Serikali.
Mwisho.
from MPEKUZI https://ift.tt/2sbyF5B
via IFTTT
No comments:
Post a Comment