Tuesday, January 26, 2021

Waziri Mkuu Majaliwa ashiriki mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia (CCM) mkoa wa Manyara Martha Umbulla


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameshiriki mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia (CCM) mkoa wa Manyara Martha Umbulla na ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wamuezi kwa kuayaendeleza mambo mema ayaliyofanya katika kipindi cha uhai wake.

Mazishi hayo ya Martha yamefanyika leo (Jumanne, Januari 26, 2021) nyumbani kwake katika kijiji cha Dongobesh wilayani Mbulu mkoa wa Manyara. Mbunge huyo alifariki Jumanne, Januari 21, 2021 katika Hospitali ya HCG Mumbai, India alikokuwa anatibiwa.

“Nimekuja kuungana nanyi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa mume wa marehemu, watoto na familia kufuatia msiba mzito wa kuondokewa na mpendwa wetu Mheshimiwa Umbulla.”

Waziri Mkuu amesema tukio hilo ni zito na ni ngumu kuishi nalo kwa sababu marehemu Martha aliishi vizuri na wabunge wenzake na pia katika kipindi chote cha ubunge wake aliishauri vizuri Serikali. “Kifo chake ni pigo kubwa kwa Serikali, hivyo itaendelea kuthamini na kuuenzi mchango mkubwa alioutoa.”

Amesema jambo la muhimu kwa sasa ni kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema. “Mume wa marehemu, watoto, ndugu, jamaa, wabunge na wananchi wa Mkoa wa Manyara namuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema Bunge limempoteza mtu muhimu sana na litamkumbuka marehemu Martha kwa mchango mkubwa alioutoa enzi za uhai wake. Amesema marehemu Martha alikuwa mlezi kwa wabunge wapya wanaoingia bungeni.

Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akizungumza kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Manyara amesema marehemu amewafundisha mambo mengi ikiwemo kufanya kazi kwa bidii, upendo, uvumilivu, kusamehe na kuomba msamaha pamoja na kumcha Mwenyezi Mungu. “Dada Martha hakuwa mbunge wa kawaida.”

Awali, akisoma wasifu wa marehemu mtoto wa kwanza wa marehemu Innocent Umbulla alisema Martha Umbulla alizaliwa Novemba 10, 1955 katika kijiji cha Dongobesh wilayani Mbulu na alikuwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wanne.

Alisema mwaka 1963 hadi 1969 alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Dongobesh na baadaye aliendelea na masomo ya sekondari katika shule ya wasichana ya Korogwe mwaka 1970 hadi 1973. Mwaka 1974 hadi 1975 alisoma shule ya sekondari ya wasichana ya Tabora.

“Mwaka 1976 alihudhuria kwa mujibu wa sheria mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Ruvu na mwaka 1977 hadi 1979 alisoma stashahada ya kilimo katika Taasisi ya Kilimo Ukiliguru Mwanza. Mwaka 1989 hadi 1990 alisoma shahada ya juu katika chuo cha Reading , Uingereza na mwaka 2000 hadi 2002 alisoma shahada ya uzamili katika fani ya usimamizi wa biashara nchini Netherland.

Alisema marehemu alifanyaka kazi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukufunzi katika Taasisi ya Kilimo Ukiliguru, , Mkufunzi Mbobezi wa Maafisa Ugani katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa wilaya ya Kongwa na Kiteto.

Innocent alisema “Mama alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Manyara kuanzia mwaka 2005 hadi umauti unamfika. Mama alikuwa na upendo mkubwa kwa jamii aliyoitumikia. Kipekee aliwapenda sana wanawake na alimiani wanamchango mkubwa katika kuendeleza jamii nan chi kwa ujumla.”

Ibada ya mazishi ilifanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu Jimbo la Dongobesh na kuongozwa na Msaidi wa Askofu  wa Jimbo la Mbulu Mchungaji John Nade ambaye aliwasisitiza waombolezaji wajiandae kukutana na Mwenyezi Mungu kwa sababu hawajui siku wala saa.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI https://ift.tt/2KPspKB
via IFTTT

No comments:

Post a Comment