Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega amewaelekeza viongozi wa Umoja wa Vituo na Shule za kuvumbua, kulea na kuendeleza Michezo kwa Watoto na Vijana Tanzania (TASCA) kufanya marekebisho ya Katiba yao ili waweze kutambulika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kunufaika na fursa zake za kuendeleza programu mbalimbali za wa watoto na vijana.
Akifanya mazungumzo na viongozi hao Dar es salaam Naibu Waziri Ulega amewashauri viongozi hao kujisajili vitambulike kama Umoja wa Kuvumbua, Kulea na kuendeleza Mpira wa Miguu kwa Watoto na Vijana Tanzania (TAFOCA) ili waweze kutambulika na TFF na kunufaika na fursa zake.
“Sasa usajili wa TASCA unawatambua kama Umoja wa Vituo na Shule za Kuvumbua, Kulea na kuendeleza Michezo kwa Watoto na Vijana jambo linalowakosesha fursa ya kutambuliwa na TFF,” alisema Naibu Waziri Ulega
Aidha, Naibu Waziri Ulega amewahakikishia viongozi wa TASCA kuwa Serikali imepokea mawazo yao yote ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya kuboresha Kanuni za BMT ili kuweka utaratibu wa wachezaji wa timu B za Vijana za vilabu vya Ligi Kuu na wanaofanya vizuri kwenye timu za Taifa za U17 na U20 wapewe nafasi ya kucheza kwenye michuano ya ligi Kuu badala ya kubakia kwenye timu za vijana za vilabu hivyo ili kuwaongezea uzoefu na kuendeleza vipaji vyao kwa manufaa ya Taifa.
Pia Naibu Waziri Ulega amewaahidi viongozi wa TASCA kuwa Serikali italifanyia kazi ombi lao la kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma kama Vyuo na Shule ili kutumia miundombinu iliyopo katika Taasisi hizo kwa shughuli mbalimbali za kukuza na kuendeleza michezo nchini.
from MPEKUZI https://ift.tt/3rlvTEz
via IFTTT
No comments:
Post a Comment