Monday, April 19, 2021

Mkuu wa Shirika la Reli Misri ajiuzulu....Ni Baada ya Ajali Nyingine Kuua Zaidi ya Watu 11


Mkuu wa Shirika la Reli la Misri amejiuzulu baada ya kutokea ajali ya tatu ya treni nchini humo katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja.

Ajali hiyo iliyotokea jioni ya jana katika mji wa Banha katika mkoa wa Qalyubia, imepelekea kuuawa watu wasiopungua 11 na kujeruhi wengine 98. 


Waziri wa Usafirishaji wa Misri, Kamel al-Wazir amesema kuwa wahusika wote wa ajali hiyo watachukuliwa hatua kali.

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Misri vinasema idadi ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo imefikia watu 16. Taarifa zinasema kuwa, uchunguzi wa awali umebaini kuwa, kasi kubwa ndiyo sababu ya ajali hiyo.


Katika miezi ya karibuni Misri imekuwa ikishuhudia ajali mbaya za treni zilizosababisha vifo vya makumi ya watu. Tarehe 15 mwezi huu wa Aprili watu 15 walijeruhiwa baada ya treni kuacha njia yake karibu na mji wa al Minya huko kaskazini wa Cairo. 


Tarehe 26 mwezi Machi pia watu wasiopungua 32 walifariki dunia katika ajali ya treni iliyotokea kwenye mkoa wa Sohag huko kusini mwa Misri huku wengine zaidi ya 160 wakijeruhiwa. 

 

-Parstoday



from MPEKUZI https://ift.tt/2Qd55ZS
via IFTTT

No comments:

Post a Comment