Wednesday, April 21, 2021

Tunzaa yazindua app ya kuimarisha tabia za kifedha kwa wanunuaji na wauzaji wa huduma na bidhaa


Kigamboni, Dar es salaam/Aprili 21, 2021 - Tunzaa yatangaza kuzindua jukwaa lake jipya la kukuza tabia chanya za matumizi ya kifedha kwa vijana wa Kitanzania kupitia teknolojia (simu za rununu yaani ‘smart phones’). 
 
Tunzaa imeundwa kuwezesha malipo ya bidhaa na huduma kwa kiwango kidogo cha pesa kwa kasi ya mtumiaji mwenyewe moja kwa moja kutoka kwenye simu zao na kuifanya iwe rahisi kufikia malengo na mipango yao.
 
"Fikiria safari ya kwenda Zanzibar na mtu unayemjali, sasa tunakupa kifaa cha kukufikisha kwenye lengo hilo kwa kulipia huduma polepole kwa kasi yako mwenyewe na programu za Tunzaa", alisema Jasmine Lupatu (Watu na Washirika, Tunzaa Fintech). 
 
Tunzaa huwapa watumiaji uwezo wa kufuatilia kila pesa wanayoweka kando kwa lengo maalum  kwa wakati halisi (mfano unataka kununua TV mpya kabisa, au iPhone/Samsung Galaxy ya hivi karibuni au kusafiri kwenda Zanzibar).
 
Watumiaji wa Tunzaa wanapata bidhaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara kuanzia vifaa vya nyumbani, safari, Runinga, Mashine za kufulia, Friji, Simu za Mkononi, kompyuta na nyinginezo zinazowapa watumiaji njia rahisi ya kulipia huduma na bidhaa na kufuatilia matumizi yao.
 
Tunzaa inawazawadia watumiaji na pointi ambazo zinaweza kutumika katika maduka makubwa, migahawa au biashara zingine ili kuhimiza tabia chanya za matumizi ya fedha.

 

Akizungumza na waandishi wa habari kupitia simu asubuhi ya leo, mwanzilishi wa Tunzaa Fintech, Ng’winula Kingamkono ameongeza ”Safari ya kutengeneza bidhaa hii ni tofauti na nyingine yoyote tuliyowahi kufanya. Tazama, kwenye Tunzaa tunahakikisha tunakidhi mahitaji ya soko sahihi na tumekuwa tukijishughulisha na utengenezaji wa Tunzaa kwa utulivu kwa miezi kadhaa iliyopita tukijaribisha mifano (‘prototype) zaidi ya mitano bidhaa hiyo hadi sasa."
 
Kwa sasa huduma hii inapatikana kwa mualiko maalum tu ikiwa kwenye majaribio, Tunzaa inakaribisha idadi ndogo ya watumiaji ili kuweza kujifunza zaidi na kuboresha uzoefu wa watumiaji na watu wanaopenda wanaweza kujisajili kupata toleo la beta (majaribio) la Tunzaa kwa kutembelea wavuti yao ya www.tunzaa.co.tz.  
 
Kuhusu Mwanzilishi wa Tunzaa Fintech

Ng’winula Kingamkono ni mwanzilishi wa Tunzaa Fintech mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika utengenezaji wa programu (‘software development’). 
 
Kingamkono ni mwanateknolojia na mchambuzi wa Mifumo ya Taarifa (‘Information Systems Analyst’) aliyewahi kushinda tuzo mbili za FinDisrupt (2016) zilizotolewa na Financial Sector Deepening Trust (FSDT, Tanzania) kwa ‘Customer Pitch’ bora na ‘Most Innovative Product Development’ (Arusha, 2016). 
 
Mnamo mwaka 2015, Kingamkono (kupitia programu yake ya Guumzo) alichaguliwa kwenye tuzo za Apps Africa (Cape Town, 2015) na alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa bidhaa za Kiteknolojia wa kwanza kuiwakilisha Tanzania katika Slush (Helsinki, 2015) na Pivot East (Nairobi, 2015 ). 
 
Kingamkono alionesha kifaa cha IoT kinachokusanya data za barabarani wakati wa Wiki ya Ubunifu wa Uholanzi (‘Dutch Design Week’) (Eindhoven, 2016) na alihudhuria mafunzo ya Swedish Institute juu ya Udumishaji wa Biashara (Stockholm, 2016/2017). Kingamkono ni mhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Tanzania) na kwa sasa ni mwanzilishi na Meneja wa Maendeleo ya Biashara huko Ellipsis Digital.
 
Ellipsis Digital ni kampuni ya kimataifa ya utengenezaji wa programu za komputa na simu ambayo inayofundisha (bure) na inaajiri wahandisi wa programu za kompyuta na simu ili kutengenezaa programu hizo kwa ajili ya biashara, mashirika na kampuni.
 
Ellipsis Digital inaendelea kujenga programu kwa wateja wa Tanzania, Uingereza, Austria, Israeli na nchi zingine ambazo zimehudumia wateja ikiwa ni pamoja na Benki ya Kitaifa ya Biashara (NBC Ltd), Taasisi ya Bima ya Tanzania (IIT), Uongozi Institute, Popcorn Email, Careers Calendar na nyinginezo. Ellipsis Digital pia inaandaa watengenezaji wa programu nchini Tanzania kupitia Developers Outreach Program.
 
Developers Outreach Program ni mpango wa mafunzo ulioundwa kuwawezesha vijana na kujifunza namna ya kuandaa na kutengeneza programu za simu na kompyuta (yaani ‘software development’) na ujuzi wa ushirikiano wa kibiashara. Mpango huo umefikia zaidi ya wanafunzi 100 tangu kuzinduliwa kwake mnamo 2019 ikiwa na dhamira ya kufundisha zaidi ya watengenezaji wa programu 100,000 kutoka Afrika ifikapo 2030.
 


from MPEKUZI https://ift.tt/3sCHQ8W
via IFTTT

No comments:

Post a Comment