Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Dodoma
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ametaka watumishi wa Wizara hiyo kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu yao hatua inayoboresha utendaji kazi na kufikia malengo ya Serikali.
Waziri Bashungwa amesema hayo leo Aprili 17, 2021 Jijini Dodoma katika kikao cha wafanyakazi wa Wizara hiyo chenye lengo la kuwakaribisha viongozi wapya pamoja na kufanya kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo.
“Wizara hii ni ya furaha kulingana na sekta zake, nasisitiza upendo, uaminifu na ushirikiano na kuchapa kazi kwa weledi na kuongeza ubunifu katika kazi tunazofanya kwa maslahi ya Taifa hili” amesema Waziri Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa amesisitiza kuwa Viongozi na watumishi wa Wizara hiyo ni lazima kufanya kazi kwa bidii na jitihada katika maeneo yao ya kazi kwa kuungaanisha nguvu kwa kuwa wanasifa kwenye nafasi zao ili Wizara hiyo iweze kufika mbali zaidi katika kuwatumikia Watanzania.
“Naamini katika ushirikiano, sisi viongozi wenu tunachotarajia ni kuona mnaendelea kuwa wazalendo, wachapakazi, wabunifu na kuwa watu mnaowekeza katika bidii ya utendaji na sio majungu, fitna na uzembe kazini” amesema Waziri Bashungwa.
Waziri Bashungwa ameongeza kuwa Wizara yake tayari imetekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kuhusu kufungulia Vyombo vya Habari hususan Online TV ambapo maagizo hayo yameyatekeleza kwa kushirikiana na Wizara ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano kupitia Mamlaka ya Mawasilano Tanzania (TCRA).
Kwa upande wake Naibu Waziri katika Wizara hiyo Mhe.Pauline Gekul amemshukuru Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo na kuahidi kumpa ushirikiano na kutoa matokeo anayotarajia.
Naibu Waziri Gekul amewasisitiza watumishi hao kushirikiana katika kufanya kazi kwasababu Wizara hiyo ni nyeti na inagusa maisha ya watu kupitia sekta zake na kuikumbusha jamii kuzingatia utamaduni pamoja na kuimarisha na kuenzi mila na desturi za nchi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi amekuwajulisha watumishi hao kuwa Bajeti ya Wizara inaendelea kuongozeka mwaka hadi mwaka ikiwemo Bajeti ya Maendelo pamoja na ile matumizi mengine.
Kwa mwaka ujao wa fedha wa 2020/2021 Wizara inatarajia kuwa na ongezeko la Bajeti ya Fedha za maendeleo kufikia Bilioni 20 kutoka shilingi Bilioni 7.7 Mwaka uliopita na fedha za matumizi mengine zimeongezeka na kutoka Shilingi Bilioni 11 kwa mwaka 2019/2020 na inatarajiwa kufikia Bilioni 14 kwa mwaka ujao wa Fedha 2020/2021 amabazo zimetengwa kutekeleza majukumu ya Wizara hiyo.
from MPEKUZI https://ift.tt/3dp2fty
via IFTTT
No comments:
Post a Comment