Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mstaafu) Mheshimiwa Dkt. Steven J. Bwana amezitaka Kamati za Uchunguzi zinazoundwa kuchunguza tuhuma wanazokabiliwa nazo watumishi wa umma kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuziwezesha Mamlaka za Nidhamu kutoa uamuzi wa haki.
Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana amesema haya wakati wa Mkutano wa Nne kwa mwaka 2020/2021 wa Tume ya Utumishi wa Umma unaoendelea kufanyika Jijini Dar es Salaam.
“Kamati za Uchunguzi zinazoundwa na Mamlaka za Nidhamu zina wajibu wa kufanya kazi yake kama inavyoelekezwa katika Hadidu za Rejea wanazopatiwa. Kamati hizi zinatakiwa kufanya kazi yake kwa weledi mkubwa ili kuthibitisha au kutothibitisha tuhuma, makosa wanayotuhumiwa nayo watumishi ili kuondoa utata. Baadhi ya Kamati hizi zinashindwa kufanya kazi yake ipasavyo na kusababisha baadhi ya Mamlaka za Nidhamu kujielekeza vibaya katika kuhitimisha mashauri ya nidhamu” alisema Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana.
Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana alisema katika kupitia rufaa na malalamiko yanayowasilishwa mbele ya Tume baadhi ya mashauri yamekuwa yakiamuliwa na Tume kuwa yaanzishwe upya na Mamlaka za Nidhamu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo, hii ni kwa sababu Kamati za Uchunguzi zimeshindwa kutoa uthibitisho, kuondoa utata kama kweli makosa anayotuhumiwa kutenda mtumishi yamethibitika.
“Ni muhimu sana kwa Kamati za Uchunguzi kuzitumia Hadidu za Rejea wanazopewa kuwawezesha kutoa ripoti nzuri. Wanapaswa kusema katika ripoti zao yale waliyoyaona na kuyabaini kwa ukweli. Watambue kazi yao kubwa ni kuthibitisha au kutothibitisha tuhuma ili haki iweze kutendeka” alisisitiza Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana.
Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Immaculata Ngwale alisema Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu zinapaswa kuwa makini wakati wa kushughulikia masuala ya Nidhamu kwa Watumishi walio chini yao.
“Hadidu za Rejea wanazopatiwa Kamati ya Uchunguzi zinapaswa kulenga katika kupata matokeo, kuchunguza tuhuma, kuthibitisha au kutothibitisha makosa ili haki itendeke. Pale Mamlaka za Nidhamu zinapoona Hadidu za Rejea ilizotoa zina upungufu ni muhimu sana zirejee Taratibu na Miongozo iliyopo na lengo liwe ni kuhitimisha mashauri haya kwa haki” alisema Mheshimiwa Ngwale.
Mkutano wa Tume utaendelea kesho kwa mujibu wa ratiba na utahitimishwa tarehe 02 Julai, 2021.
from MPEKUZI https://ift.tt/3wb3BhE
via IFTTT
No comments:
Post a Comment