Friday, August 13, 2021

Chanjo ya Corona Sasa ni Ruksa kwa Watanzania Wote

 


NA WAMJW- DSM
KATIBU MKUU Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi ametoa ruksa kwa wananchi wote wenye zaidi ya miaka 18 kupata huduma ya Chanjo, huku akielekeza makundi ya kipaumbele yapewe nafasi ya upendeleo wakati huduma hiyo ikiendelea.

Prof. Makubi ametoa agizo hilo jana wakati alipotembelea kituo cha kutoa huduma za chanjo ya COVID-19 kilichopo katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

“Chanjo zipo, na wananchi wote ambao wana umri kuanzia miaka 18 na kuendelea wanakaribishwa kwenye vituo vyetu ambavyo vipo zaidi ya 550 nchi nzima, ila ambacho tunaendelea kusisitiza, wakiwepo wazee na wale wenye magonjwa sugu watangulie kupewa huduma” amesema Prof. Makubi

Aliendelea kusema kuwa, wale ambao walikuwa wakisita kwenda kupata huduma ya Chanjo kwa kigezo cha kutokuwa kwenye makundi ya kipaumbele waondoe shaka na kwenda kupata huduma hiyo, kwani Serikali imeshajipanga kuwahudumia wananchi wa makundi yote.

Amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya leo imeanza kutoa huduma ya vyeti vya chanjo kwa njia ya elektroniki yenye ‘QR Code’ na kuachana na mfumo wa karatasi ngumu (hard copy) ili kudhibiti mtu yeyote anayedhamiria kufoji cheti ama kupata kwa njia ya udanganyifu.

“Tulipoanza hili zoezi tulikuwa tunatoa vyeti kwa njia ya karatasi ngumu, lakini sasa tunabadilisha kutoka kwenye mfumo wa karatasi ngumu (hard copy) kwenda kwenye mfumo wa elektroniki kupitia njia ya tehama na leo tumeshaanza hilo ” amesema.

Alisisitiza kuwa, kuanzia wiki ijayo wote walipewa cheti kwa njia ya karatasi ngumu (hard copy) wataitwa kwa njia ya simu katika maeneo waliopata huduma hiyo ya chanjo ili kupewa vyeti vilivyo kwenye mfumo wa elektroniki au watatumiwa kiunganishi (link) kwenye simu na kui print ili kupata kadi hiyo.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Tehama Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Silvanus Ilomo amesema kuwa, baadhi ya watu waliopata huduma ya chanjo na kupewa vyeti vya karatasi ngumu (hard copy) leo tayari wameshaanza kubadilishiwa na kupewa vyeti vya elektroniki.

Akieleza sifa za Cheti hizo, Bw. Ilomo amesema kuwa, cheti hicho kina QR Codes ambayo imetengenezwa kwa njia ya mfumo uliotengenezwa na Wataalamu wa Wizara ya Afya, na popote utapoenda Duniani kwa kutumia cheti hicho inaonesha cheti hicho kimetolewa ma Wizara ya Afya Tanzania.

Alisisitiza kuwa tayari, Wizara ya Afya imeshatoa mafunzo kwa Wataalamu mbalimbali nchini wa namna ya kutumia mfumo huo wa TEHAMA ambao unakusanya taarifa za wananchi waliochanja ili kupata vyeti hivyo vya elektroniki.


from MPEKUZI https://ift.tt/3AFPUtO
via IFTTT

No comments:

Post a Comment