Sunday, August 8, 2021

Naibu Waziri Mabula Ahimiza Uwajibikaji Sekta Ya Ardhi


 Na Munir Shemweta, MUSOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka watendaji wa sekta ardhi katika halmashauri na Manispaa za mkoa wa Mara kuwajibika kwa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanatoa hati kwa wamiliki wa ardhi pamoja na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi .

Akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara, Dkt Mabula alisema ufanyaji kazi kwa kujituma kwa watumishi wa sekta hiyo itaiwezesha wizara ya ardhi kuongeza kasi ya utoaji hati na wakati huo kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, kwa sasa katika mkoa huo Mara kasi ya utoaji hati za ardhi pamoja na makusanyo yatokanayo na kodi ya ardhi hairidhishi na juhudi kubwa zinahitajika katika kutoa hati na kuhamasisha wamiliki kulipa kodi ili serikali iweze kupata fedha za kuendesha shughuli zake mbalimbali.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mara Bi. Hapiness Mtutwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 uliweza kukusanya shilingi bilioni 1.065 sawa na asilimia 23 katika malengo ya bilioni 4 huku mwaka wa fedha 2020/2021 ukikusanya bilioni 1.7 sawa na asilimia 47.5 kati ya malengo bilioni 3.7.

‘’Maelekezo yangu mkafanye kazi kwa bidii  katika wilaya zenu na nikikuta mtendaji wa sekta ya ardhi hafanyi haya ninayoelekeza basi  ujue wewe hutufai’  alisema Dkt Mabula

Mkurugenzi Msaidizi idara ya Maendeleo ya makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Imaculata Senje aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi hasa wale wa Mipango Miji kuwa wabunifu kwa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa maeneo yao kupimwa.

‘’Kuna miji midogo inakuwa kwa kasi katika maeneo yenu na inawezekana kama Afisa Mipango Miji ukasema huna kazi lakini unaweza kuanza kwa ktuoa elimu kwa mtu mmoja mmoja ukieleza umuhimu wa eneo lake kupangwa na kupima na kumilikishwa’’ alisema Bi. Senje.

Naye Afisa Kodi Kutoka Wizara ya Ardhi Rehema Kilonzo aliwaeleza watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Mara kuhakikisha wanayajua na kufuatilia kwa karibu madeni ya wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi na kubainisha kuwa, pamoja na Wizara kuelewa changamoto zilizopo kwenye mfumo lakini bado watendaji hao wana nafasi ya kujua madeni halisi ya wadaiwa na hivyo kuwafanya kuwa katika sehemu salama kwenye utendaji wao.


from MPEKUZI https://ift.tt/3rYvGZi
via IFTTT

No comments:

Post a Comment