Monday, June 13, 2022

Andaeni Mpango Kazi Unaolenga Kuwanufaisha Wananchi: Msajili Mkuu


Na Mary Gwera, Mahakama

MSAJILI Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewataka Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni kuandaa mpango wa namna ya kutekeleza utendaji kazi utakaolenga kumridhisha mteja kulingana na huduma zinazotolewa na Kituo hicho.

Akizungumza na Watumishi wa Kituo hicho mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akifunga Mafunzo ya Huduma kwa Mteja, Mhe. Wilbert Chuma alisema kuwa ana imani kuwa mafunzo waliopata Watumishi hao yatawasaidia kutokufanya kazi tena kwa desturi na mazoea ya awali bali kufanya kazi kwa weledi.

 “Nina imani kuwa Wananchi wanaokuja kupata huduma katika Mahakama Jumuishi wapate huduma zilizo bora, hivyo ni muhimu kuzingatia mafunzo haya kwa kuleta tija, na hayatakuwa na maana kama hamtayatekeleza kwa vitendo,” alisema Mhe. Chuma.

Msajili Mkuu aliongeza kwa kuwataka pia watumishi hao kutekeleza maelekezo ya viongozi hususani matumizi ya TEHAMA katika kusikiliza mashauri kwa njia ya runinga (Video conferencing) na maelekezo ya Jaji Mkuu kupitia kauli mbiu ya Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho Kuelekeza Mahakama Mtandao na kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa.

“Kufanyika kwa mafunzo haya kutakuwa chachu ya kuboresha huduma zitakazotolewa na Mahakama Pamoja na wadau katika Mahakama hii Jumuishi ili kuleta maana halisi ya uanzishwaji wake,” alisisitiza.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) ambayo pia yalifanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Temeke yalihudhuriwa na Watumishi wote wa Vituo hivyo pamoja na wadau wa Mahakama waliomo katika vituo hivyo.

Mada zilizotolewa ni pamoja na utoaji wa huduma ya kwanza, maadili ya msingi na utamaduni wa Mahakama, Mkataba wa huduma kwa mteja, maadili yaliyobinafsishwa ndani ya Mahakama ya Tanzania, usawa katika taaluma na muonekano wa mtu, masuala ya kisaikolojia kanuni za maadili yanayofaa na huduma kwa mteja kuendana na viwango vya IJC Vituo Jumuishi vya Utoajia Haki (IJC).



from MPEKUZI https://ift.tt/PjXNzhc
via IFTTT

No comments:

Post a Comment