Friday, October 18, 2019

Benki Ya Dunia Kuijaza Zanzibar Dola Za Marekani Milioni 150 Kukuza Utalii Na Ustawishaji Miji Zanzibar.

Na Eva Valerian na Ramadhani Kissimba, Washington DC
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatarajia kupata dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia-WB zitakazotumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya kukuza Utalii na kustawisha miji katika visiwa hivyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Bw. Khamis Omar alisema Jijini Washington DC kuwa Benki ya Dunia imekuwa mshirika mzuri wa maendeleo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutokana na misaada mbalimbali wanayoitoa katika kutekeleza miradi yao ya maendeleo.

Bw. Omar alisema Benki hiyo imesaidia kufadhili ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara zinazoingia mijini, Uwanja wa Ndege wa Zanzibar pamoja  na bandari.

Aidha, alisema Benki hiyo imesaidia zaidi katika ujenzi wa Uwanja wa ndege, kwa kujenga sehemu ya maegesho ya ndege, njia ya kutua na kurukia ndege na njia ambazo ndege zinapita kabla ya kuingia kwenye sehemu ya kurukia (runway).

“Pia Benki hii imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya Elimu Visiwani Zanzibar ukiwemo mradi wa kukuza matokeo na kuongeza ufaulu wa  wanafunzi katika shule za Zanzibar” alisema Bw. Omar

Alieleza kuwa kwa sasa wanatekeleza mradi mkubwa wa ustawishaji wa huduma za mijini ambao unafadhaliwa na Benki ya Dunia, na mradi huo utasaidia kuboresha huduma muhimu katika Miji ya Zanzabar ikiwa ni pamoja na kuongeza vivutio vya utalii.

“Mradi huu umekamilika katika awamu ya kwanza,na awamu ya pili itatekelezwa baada ya Benki hiyo kuridhia na kutoa idhini ya utekelezaji wa mradi huo ambapo idhini hiyo  inatarajiwa kutolewa mwezi Aprili, 2020” alisisitiza Bw. Omar 

Katibu Mkuu -Wizara ya Fedha na Mipango ameishukuru Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa kwa ushikiano mzuri wanaouonyesha katika kusukuma maendeleo ya Visiwani Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla.             

Awali Waziri wa Fedha na Mipango, wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Balozi Mohamed Abdiwawa alisema lengo la kushiriki katika Mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia-WB na Shirika la Fedha la Kimataifa -IMF ni kujadiliana na vyombo hivyo vya fedha duniani kuhusu miradi inayotekelezwa kwa sasa na kuangalia mustakabali wa utekelezaji wa miradi ambayo inategemewa kutekelezwa kwa siku zijazo.

Mwisho




from MPEKUZI https://ift.tt/31rY5b2
via IFTTT

No comments:

Post a Comment