Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameahirisha sherehe za maadhimisho siku ya Makazi Dunia na kuagiza fedha iliyopangwa kwa ajili ya sherehe hiyo shilingi milioni 23 kutumika kuboresha mfumo wa mapato na utoaji huduma za ardhi.
Katika salamu zake za siku ya Makazi Duniani yenye kauli mbiu ‘Matumizi ya Teknolojia Bunifu Kubadili Taka kuwa chanzo cha Mapato’ Lukuvi ametaka maadhimisho ya mwaka huu kutofanyika sherehe na badala yake yatumike kutafakari kauli mbiu ya na kujipanga upya kutekeleza agizo la rais alilolitoa muda mrefu la kuwataka wananchi kujitolea kufanya kazi za usafi katika maeneo ya miji na wanayoishi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inaelekeza kutafakari kwa kina namna changamoto ya uwepo wa taka mijini kuwa fursa ya kujiongezea kipato kwa kutumia teknolojia rahisi.
Alisema, mwaka huu inaelekezwa kuingia kwa undani zaidi kutumia ubunifu kubadili taka kuwa mtaji na kuongeza kipato kwa wananchi bila kuathiri afya za wakazi wa mijini na mazingira na hatimaye kupunguza gharama za udhibiti taka.
‘’Mamlaka za miji zina wajibu wa kukusanya taka kama mojawapo ya huduma wanazotakiwa kuzitoa kwa wananchi na kwa upande mwingine wananchi wanao wajibu wa kulipia huduma hiyo kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha mamlaka za mitaa’’ alisema Lukuvi.
Aliwaasa wananchi kuepuka kutupa taka kando ya mito , maeneo ya wazi , barabarani na katika mitaro ya maji ya mvua kwa kuwa kufanya hivyo kunasababisha uharibifu wa mazingira , kuziba kwa mitaro ya maji ya mvua na kutengeneza mafuriko.
Aidha, ameaalika wadau wote wenye teknolojia rahisi ya kuchakata taka ngumu kushirikiana na mamlaka za miji nchini ili kutumia ujuzi huo kupambana na changamoto ya wingi wa taka ngumu na kwa njia hiyo wataweza kutengeneza ajira kwa jamii huku miji ikiendelea kuwa safi na afya za wananchi kuimarika.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Makazi Duniani (UN Habitat) kupitia azimio Namba 40/202 la Baraza la Umoja wa Mataifa la mwezi Desemba mwaka 1985 limetenga jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba ya kila mwaka kuwa siku ya Makazi Duniani. Kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yalifanyika jijini Nairobi, Kenya mwaka 1986. Mwaka huu Maadhimisho hayo yanafanyika kimataifa katika jiji la younde Cameroun.
from MPEKUZI https://ift.tt/30UDMD9
via IFTTT
No comments:
Post a Comment