Monday, October 7, 2019

Mvua Yaua Watu Watano Jijini Mbeya

Kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Oktoba 06, 2019 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya imesababisha vifo vya watu watano na uharibifu wa makazi ya watu katika maeneo ya Iyunga Jijini Mbeya.

Mnamo tarehe 06/10/2019 majira ya saa 17:00 jioni huko katika maeneo ya Mwasanga, Kata ya Mwasanga, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, watu watatu waliofahamika kwa majina ya 1. AJUAYE JAMES @ SANGA [25] fundi ujenzi na Mkazi wa Mwasanga na 2. MARIA JUMA MWASHAMBWA [25] Mkazi wa Uyole na 3. ANGELA SOLO [15] Mkazi wa Mtaa wa Reli – Tembela wamefariki dunia baada ya kusombwa na maji wakati wakivuka darajani baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha kuvunjika kwa daraja la Mwasanga na kuwasomba baadhi ya watu wakiwepo marehemu.

Mwili wa marehemu MARIA JUMA MWASHAMBWA umepatikana leo Oktoba 07, 2019 majira ya saa 07:30 asubuhi pembezoni mwa daraja la Iyunga wakati mwili wa marehemu ANGELA SOLO umepatikana eneo la Utengule ndani ya Mto Nzovwe baada ya jana kupatikana na taarifa za baadhi ya watu waliokuwa wakivuka daraja la Mwasanga kusombwa na maji.

Ufuatiliaji unaendelea kuangalia kama kuna watu wengine wamesombwa na maji. Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Sambamba na hilo, mnamo Oktoba 06, 2019 majira ya saa 18:00 jioni huko eneo la Mbata, Mtaa wa Iyela one, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyung, Jijini Mbeya, watoto wawili waliofahamika kwa majina ya JONATHAS BARAKA MWANGISI [3] na IBRAHIM EFRAHIM [2] wote wakazi wa Mbata Relini wamefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye shimo lenye maji ambalo lilichimbwa udongo kwa ajili ya kufyatulia tofali lakini halikufukiwa hivyo kufuatia mvua iliyonyesha jana shimo hilo lilijaa maji.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya. Upelelezi unaendelea.

Aidha kufuatia maafa hayo yaliyosababisha na mvua kubwa iliyonyesha jana, Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ALBERT CHALAMILA imetembelea na kukagua eneo la daraja la Mwasanga pamoja na maeneo mengine yenye madaraja kama vile Ivumwe na Iyunga na kutoa rai kwa wakazi wa maeneo hayo kuwa makini hasa wakati wa kuvuka maeneo yenye maji mengi pamoja na kuimarisha ulinzi kwa watoto wao.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa rai kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya kuchukua tahadhari juu ya mvua na mito inayowazunguka. 

Mvua zinaponyesha msivuke au kufanya shughuli zozote katika maji kwa sasa kikosi maalum cha Polisi kinapita kwenye maeneo yote kuhakikisha usalama wa wakazi wote na madhara yaliyojitokeza yanaratibiwa. Natoa rai pia kwa kamati za maafa za Kata chini ya mtendaji wa Kata kufuatilia usalama wa eneo lake na kupeleka taarifa kwa Mkuu wa Polisi Wilaya [OCD] kupitia kwa Polisi Kata. Kila mmoja awe mlinzi katika muda huu.

Ujenzi mpya wa madaraja unaendelea/unafanywa na Serikali kupitia uratibu unaofanywa na Mhe. Mkuu wa Mkoa.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawapa pole familia zote zilizopotelewa na ndugu zao 05, wapate nguvu katika kipindi hiki cha majonzi.


from MPEKUZI https://ift.tt/33aNId0
via IFTTT

No comments:

Post a Comment