Monday, October 7, 2019

Mbowe Amlilia Mtunzi wa Wimbo wa "CHADEMA People’s Power”

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Sanaa ya chama hicho, Fullgency Mapunda (Mwana Cotide).

Mwanacotide ambaye pia ni mtunzi na muimbaji wa nyimbo mbalimbali za chama hicho zikiwamo nyimbo maarufu kama vile Chadema People’s Power na Mafisadi kwa heri, alifariki usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya St. Monica, Manzese jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika ukurasa wake wa Facebook, Mbowe amemuelezea msanii huyo kuwa atakumbukwa kwa mazuri yake.

“Nimepokea kwa huzuni kubwa kifo cha Kamanda wetu Fullgence Mapunda Mwanacotide, ni mapema sana Kamanda umeondoka, kimwili haupo nasi lakini utaishi kwenye mioyo ya walio wengi kupitia muziki wako.

“Mara ya mwisho nilikutembelea hospitalini tuliongea mambo mengi, ulisema umefurahi sana kuniona, nikakwambia ni kawaida mtu anapougua binadamu wenzake kumtembelea kumjulia hali na kufarijiana, ukaniambia Chairman (mwenyekiti) wewe una mambo mengi uko busy sana, hadi kuja kunijulia hali ni heshima kubwa Chairman.

“Ulitunga nyimbo nzuri za hamasa katika chama chetu cha Chadema, ambazo zitafanya tukukumbuke kila zitakaposikika masikioni mwetu, kupitia nyimbo zako nzuri kwa chama chetu, daima uliweza kuwagusa wengi kwa njia ya muziki. Vita vizuri umepigana Kamanda na mwendo umemaliza.

“Kwa ujumla ni mengi yapo ya kukuelezea lakini kwa hatua ya sasa tunakuombea kwa Mungu aipokee roho yako na kuipumzisha mahali pema,” ameandika Mbowe.


from MPEKUZI https://ift.tt/2AOqBZV
via IFTTT

No comments:

Post a Comment