Monday, October 7, 2019

Waziri Mkuu Amuagiza Mkurugenzi Manispaa Ya Singida Awaondoe Wakusanya Mapato Watatu Walioajiriwa KINDUGU na wanatumiwa kuiba mapato.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi Manispaa ya Singida, Bw. Bravo Lyapembile awaondoe kazini watumishi watatu wanaokusanya mapato kwenye stendi ya mabasi ambao wameajiriwa kindugu na wanatumiwa kuiba mapato.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Oktoba 7, 2019), akizungumza na madiwani na watumishi wa Manispaa ya Singida pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Roman Catholic, mjini Singida.

“Kuna vijana watatu pale stendi ambao mmewaweka kindugu. Yupo Kennedy Francis (mtoto wa Mkurugenzi); Selemani Msuwa (ndugu yake diwani) na Salehe Rajab Kundya (shemeji yake diwani mwingine). Andika barua leo hii, hawa vijana waondoke kwenye hiyo kazi, na upeleke timu nyingine ya watu waaminifu,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kuna mchezo unachezwa wa kukusanya mapato lakini hayapelekwi benki na wahusika wakuu ni  mweka hazina wa Manispaa, Bw. Aminieli Kamunde na Mkaguzi wa Ndani, Bw. Ibrahim Makana.

Amewaonya watendaji wa kata wanaohusika kukusanya mapato wahakikishe kuwa kila wanapokamilisha makusanyo, wanazipeleka fedha hizo benki na kupatiwa risiti. “Kuna wakusanyaji wanaoshirikiana na baadhi ya Wakurugenzi na Waweka Hazina. Waheshimiwa Madiwani hakikisheni mnasimamia hizo mashine zinazokusanya mapato na mjue ni nani amepatiwa. Ombeni taarifa mjue nani anayo na yuko wapi.”

“Ninawasihi Mstahiki Meya na Mwenyekiti wa Halmashauri msiingie kwenye huu mkumbo kwa sababu tunataka fedha zilizokusanywa kutoka kwa wananchi zirudi kuwahudumia wananchi.”

Waziri Mkuu amekemea tabia ambayo ameikuta kwenye Halmashauri nyingine ya kubadilisha matumizi ya fedha ambako Mkurugenzi au Mweka Hazina wanawadai watendaji wa kata wawapatie shilingi milioni mbili. “Kwenye eneo hilo, msikubali kupeleka fedha mkononi kwa afisa yoyote. Ninyi pelekeni benki na mpatiwe risiti,” amesisitiza.

Amesema tabia nyingine ambayo ameikuta katika ziara hii, ni kubadilishwa kwa matumizi ya fedha na kuacha malengo kusudiwa ya fedha zilizotumwa. “Fedha inayotoka Serikali kuu ikiletwa inakuja na maelekezo mahsusi. Unakuta fedha inakuja kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, wao wanahmisha na kujilipa posho au inahamishiwa kwenye mradi mwingine.”

“Au unakuta fedha la kulipa likizo za walimu inatumika kwenye miradi ya afya, na Afisa Elimu upo. Na unajua kwamba walimu wanadai likizo zao, unaona sawa tu. Ni lazima tuchukue hatua kwa sababu huu ni mwaka wa nne wa Serikali ya awamu ya tano, na wanajua nini Serikali hii inataka. Tukiwaachia, wataendelea kufanya ubadhirifu tena na tena.”

“Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, simamieni mapato ya ndani na siyo muwe sehemu ya ulaji wa fedha za umma. Waheshimiwa Madiwani simamieni sheria inayosimamia utoaji iwa asilimia 10 ya mapato kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu ili kila mmoja apate haki yake,” alisisitiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida, Bw. Rashid Mandoa akamilishe malipo ya madiwani ambayo ni malimbikizo. “Nenda kalipe malimbikizo ya wadiwani ambayo yanafikia shilingi milioni 104,” alisema.

Pia amemtaka awasilishe kwenye mfuko wa Hifadhi ya jamii, michango ya madereva ya sh. 15,000 ambayo wamekuwa wakikatwa tangu mwaka 2015/2016 lakini haijawasilishwa. “Hawa walikuwa LAPF, wamekatwa hela zao lakini bado hazijapelekwa.”

“Watu hao pia wamekuwa wakikatwa sh. 5,500 za Bima ya Afya tangu wakati huo lakini hadi sasa michango yao haijawasilishwa na matokeo yake wakienda hospitali hawatibiwi. Hakikisha malipo yao yanaenda,” alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI https://ift.tt/2Ot1eoi
via IFTTT

No comments:

Post a Comment