Wednesday, October 16, 2019

Waziri wa Fedha Dkt. Mpango Aitaka Benki Ya Dunia Kusaidia Sekta Ya Kilimo Nchini Tanzania

Na Ramadhani Kissimba na Eva Valerian, Washington Dc
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango (Mb) ameitaka Benki ya Dunia kujikita zaidi katika kusaidia sekta ya kilimo nchini Tanzania ili kuweza kuwainua kiuchumi wakulima hasa wale wa kati na wadogo.

Dkt.Mpango aliyasema hayo wakati wa kikao cha majadiliano na timu nzima ya Benki ya Dunia ambayo inafanya kazi nchini Tanzania na wengine kutoka Makao Makuu ya Benki hiyo nchini Marekani.

Mhe.Mpango alisema katika mkutano huo  walipitia kwa pamoja utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea hivi sasa  inayofadhiliwa na Benki ya Dunia,  lakini pia walipitia na kujadili miradi ambayo inaanza kufikiriwa kwa ajili ya utekelezaji kwa mwaka utakaofuata.

‘’Moja ya vitu vilivyonifurahisha mwaka jana kwenye mjadala niliwaaomba sana kwamba hatuwezi kuendelea kuitaka Benki ya Dunia isaidie kwenye miradi mingine tu ni lazima nguvu kubwa ielekezwe pia kwenye miradi ya kilimo ambayo kwa sasa  msaada wa Benki ya Dunia katika miradi hiyo ni kidogo sana’’ alisema Dkt.Mpango.

Aidha Dkt.Mpango alielezea dhamira ya Tanzania kushirikiana na Benki ya Dunia ili kuanzisha programu itakayohakikisha kuwa tija inapatikana kwenye sekta nzima ya kilimo na mifugo, lakini pia kuweza kuyafikia masoko kwa mazao yanayozalishwa nchini, hasa yale yenye thamani kubwa duniani.

 Dkt. Mpango amefafanua kuwa Benki ya Dunia imeridhishwa na kasi ya mabdiliko inayofanyika katika sekta ya kilimo kwa maana ya uzalishaji kuongezeka, lakini vile vile  wakulima wa kati wamezidi kuongezeka.

Aidha, kuongezeka kwa maeneo ya kilimo imewafurahisha wataalamu wa Benki hiyo, ikiwa ni pamoja na  kuongezeka kwa aina ya mazao yanayolimwa   hasa yale yenye thamani kubwa ambayo yanalimwa  kwa kasi kubwa sana kuliko ilivyokuwa awali.

Pia Dkt. Mpango alisisitiza kuwa, Benki ya Dunia imeshafanya utafiti wao wa kutosha ambao umeonesha kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo kwa maana ya uzalishaji kuongezeka.

Mhe. Mpango aliishukuru Benki ya Dunia kwa kukubali tena kuleta timu ya wataalamu nchini Tanzania ambayo itakaa na sekta nzima ya kilimo na ufugaji ili kuona ni namna gani hasa Benki ya Dunia itasaidia kuinua sekta hiyo, na  kuwasaidia wakulima hasa katika matumizi ya nguvu kazi kwa upande mmoja na kuwaongezea kipato kwa upande mwingine.

Mwisho


from MPEKUZI https://ift.tt/2Bf7Kat
via IFTTT

No comments:

Post a Comment