Vijana nchini wamehimizwa kuchangamkia fursa ya mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na Serikali kupitia makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ili waweze kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya Mkoani Geita alipotembelea vikundi vya vijana ambavyo vimenufaika na mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na Halmashauri mbalimbali nchini pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya vijana, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi alitumia fursa hiyo kuwaasa vijana kuchangamkia mikopo hiyo yenye riba nafuu ili waweze kuanzisha miradi ya uzalishajimali kwenye jamii zinazowazunguka.
Alieleza kuwa, Serikali kupitia halmashauri zilizopo nchini zimekuwa na wajibu wa kutenga fedha asilimia 10 kupitia makusanyo ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu ili viweze kuanzisha miradi mipya au kuendeleza shughuli zao ambazo zitatoa fursa ya kuzalisha ajira zaidi na kuwasaidia kujiingizia kipato na hivyo kuchangia katika kuendeleza gurudumu la maendeleo.
“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea na azma yake ya kuwawezesha vijana kwa kutoa fursa nyingi kwa vijana ikiwemo mikopo yenye riba nafuu lakini vijana wamekuwa hawatumii fursa hizo zinazotolewa na serikali kwa kuanzisha miradi mikubwa itakayowawezesha kujiajiri na kuajiri vijana wenzao,” alisema Katambi
Alisema lengo la Serikali kutoa mikopo hiyo ni pamoja na kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira, hivyo kupita mikopo hiyo ambayo ina riba nafuu makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wataweza kunufaika kwa kuanzisha miradi mbalimbali ambayo itawaingizia kipato na hatimaye kuweza kujikwamua kiuchumi.
Aliongeza kuwa, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifungua rasmi Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Dodoma Novemba 13, 2020 alieleza kuwa Serikali imeongeza jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba ama yenye riba nafuu ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri na pia kupitia mifuko na Programu mbalimbali zilizoanzishwa na serikali.
Sambamba na hayo alielezea pia juu ya uwezekano wa kuiunganisha baadhi ya mifuko ili ifanye kazi kwa tija zaidi kwa kuimarisha usimamizi wa mifuko hiyo na kuhakikisha watanzania wanaifahamu.
Naibu Waziri Katambi, alitaka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuangalia namna bora ya kuanzisha mpango wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara ili kabla ya kuwapatia mkopo vijana waweze kuwajengea ujuzi utakaowasaidia kuimarisha biashara zao na kuzisimamia kwa weledi pamoja na kuwa na mbinu za kukuza biashara zao. Pia alihamaisha halmashauri kuona namna ya kuwawezesha vijana kwenye mikopo wanayoomba asilimia 50 ikawa kwa ajili ya vifaa au vitendea kazi na asilimia 50 nyingine kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli ya biashara zao watakazokuwa wakifanya.
“Kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya vijana kukosa uaminifu, wanakuja kama kikundi kukopa fedha hizo mara baada ya kuzipata wanaanza kuzitumia kwenye malengo au mipango ambayo hawakuikusudia na hivyo kushindwa kurejesha mikopo hiyo, hivyo kama kupitia mikopo waliyoomba asilimia 50 wakanunuliwa vitendea kazi au vifaa wakishindwa kuendeleza biashara itakuwa ni rahisi kwa halmashauri kuwapatia vijana wengine vifaa hivyo ambao wanaona wanaweza kufanya kazi,” alisema Naibu Waziri
Pamoja na hayo Naibu Waziri, Katambi alipongeza vikundi vya vijana alivyovitembelea ikiwemo kikundi kinachojishughulisha na uzalishaji wa Chaki kinachojulikana na jina la Rubondo na kikundi cha vijana cha Geita Youth Group kinachofatua matofali kwa hatua waliyofikia ambayo imechangia kasi ya ukuaji wa viwanda vidogo vidogo mkoani geita na ambavyo vitasaidia kutengeneza ajira na kuongeza ukuaji wa uchumi.
Aidha, Naibu Waziri Katambi amewataka vijana kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma sambamba na kutumia maarifa waliyonayo kubuni miradi mbalimbali ya uzalishajimali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Fahil Juma alieleza kuwa Halmashauri hiyo itaendelea kutoa mikopo na elimu kwa vikundi mbalimbali vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili waweze kukuza pato lao na kuongeza ajira kwa wengine zaidi.
Naye, Mnufaika wa kikundi cha Geita Youth Group, Bi. Jenifer Isaya ameishukuru Serikali pamoja na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwaamini vijana kuwa wananweza na kuamua kuwatengea mikopo hiyo yenye riba nafuu sambamba na kuwawezesha vifaa na fedha, hivyo waliahidi kuchapa kazi kwa bidi kama azma ya serikali ili warejeshe mikopo hiyo kwa wakati na kuwafanya wananchi wengine waweze kunufaika.
Mara baada ya ziara hiyo ya kutembelea vikundi vya vijana vilivyonufaika na mkopo wa asilimia nne (4) inayotolewa na Halmashauri zilizopo nchini. Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi alitembelea Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM) ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa Sheria za Kazi pamoja na kusikiliza kero na malalamiko ya wafanyakazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi.
from MPEKUZI https://ift.tt/30bKaYC
via IFTTT
No comments:
Post a Comment