Na.Catherine Sungura,Kibaha
Uchunguzi wa tathmini ya uwepo wa thamani ya fedha katika utekelezaji wa mradi wa upanuzi na uboreshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani-Tumbi umeonesha hasara ya shilingi bilioni 1.6.
Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima wakati akipokea tathmini ya awali ya mradi huo baada ya maagizo yake aliyoyatoa mnamo tarehe 24 Disemba,2020 alipotembelea hospitali hiyo na kutoridhishwa na ujenzi huo.
Katika ziara yake hiyo Dkt.Gwajima alitoa maelekezo kwa Katibu Tawala Mkoa wa kufanya tathmini ya uwepo wa thamani ya fedha katika utekelezaji wa mradi wa upanuzi na uboreshaji wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tumbi na hasara hiyo imebainika kwa kuhakikiwa kwa baadhi ya vipimo vya kazi na kuchukua sampuli chache kwa ajili ya vipimo vya kimaabara jambo lililoashiria kuwepo kwa hasara kubwa zaidi Kama ingefanyika tathmini ya kina.
“Ripoti nimeipokea na iko dhahiri kabisa mahitaji ya upanuzi na uboreshaji wa hospitali ya Tumbi yalikadiriwa kutekekezwa kwa shilingi bilioni 29 baada ya Serikali kuonyesha nia ya kusaidia ufadhiri wa mradi huo kufuatia mpango wa awali wa uongozi wa Mkoa wa mwaka 2007-2009 iliokuwa na makadirio ya shilingi bilioni 5”. Alisema Dkt.Gwajima.
Aliongeza kuwa mpaka sasa jumla ya shilingi bilioni 9.4 zimekwishatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo Kati ya shilingi bilioni 29 zilizokadiriwa ambapo bilioni 5.5 imetumika katika utekelezaji chini ya usimamizi wa Shirika la Elimu Kibaha na Katibu Tawala Mkoa na bilioni 3.9 zimehamishiwa Wizara ya Afya.
Hata hivyo Dkt. Gwajima amesema kupitia taarifa hiyo imebaini kuwepo kwa mikataba ya Wakandarasi wawili SUMA JKT na MUST Construction Bureau kinyume na Sheria namba 7 ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 pamoja na marekebisho yake mwaka 2016.
“Kutokana na mkanganyiko huo namuelekeza Katibu Tawala Mkoa kupitia Kamati yako ya tathimini mfanye tathimini ya kina ndani ya siku thelathini na kuniainishia hasara halisi kwa kurejea vipimo vya jengo zima, kutathimini na kushauri kama jengo hili linafaa kwa matumizi ya Umma pamoja na Hali ya majengo ya zamani Kama yanafaa kukarabatiwa na kutumika Tena kwa gharama stahiki”Alisisitiza Dkt.Gwajima.
Licha ya hayo Waziri huyo aliitaka Kamati hiyo pia ihakiki uhalali wa uhitaji wa shilingi bilioni 29 katika mpango wa upanuzi kwa kurejea michoro ya mpango, kuainisha sababu zilizopelekea wizara kurudia ununuzi wa mkandarasi wa awamu ya pili A na ukidhi wa kisheria katika mchakato huo wa kumnunua mkandarasi mpya na kuagiza mradi huo usitishwe na madeni yasiendelee kulipwa mpaka atakapopokea tathimini ya kina na kuelekeza vinginevyo.
from MPEKUZI https://ift.tt/3ecWYGy
via IFTTT
No comments:
Post a Comment