Friday, March 5, 2021

Waziri Lukuvi Atangaza Uhakiki Kubaini Wamiliki Wa Ardhi Hewa Nchi Nzima


Na Munir Shemweta, ILEMELA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema Wizara ya Ardhi kuanzia tarehe 1 Julai 2021 itaanza zoezi la uhakiki la kitaifa kuwatambua na kuwaondoa  wamiliki wote hewa wa viwanja nchini.


Lukuvi alisema hayo kwa nyakati tofauti tarehe 4 Machi 2021 katika ofisi za halmashauri ya Manispaa ya Ilemela alipopokea taarifa ya utekelezaji majukumu ya sekta ya ardhi na eneo la Kigoto katika kata ya Kirumba alipogawa ankara za malipo kufuatia kuhitimishwa kwa mgogoro kati ya wananchi wa eneo hilo na jeshi la polisi akiwa kwenye  ziara ya kikazi katika mkoa wa Mwanza.


“Lazima tufanye uhakiki wa wamiliki wote wa ardhi ili kuwatambua na kuondoa wamiliki hewa, katika miji kuna maeneo mengi hayajengeki kwa sababu wamemilikishwa watu ambao hawapo” alisema Lukuvi.


Alisema, katika zoezi hilo halmashauri za wilaya zitatakiwa kuandaa jedwari la kumbukumbu za wamiliki ili zoezi hilo litakapoanza taarifa mpya zitakazojumuisha kumbukumbu zilizopo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), namba za simu pamoja na taarifa za kibenki ziingizwe.


Lukuvi alisema, wapo wananchi waliojenga katika maeneo mbalimbali majina yanatofautina na wengine  majina ya kubuni lakini  hawapo tanzania na kusisitiza kuwa ikibainika viwanja vyao vitapigwa mnada na aliwaonya  watumishi wa sekta ya ardhi kutoharibu nyaraka kutokana na kuhusika kwao kwa namna moja ama nyingine katika umilikishaji.


Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi zoezi la kutambua wamiliki wa ardhi hewa halina lengo la kunyanganya viwanja bali ni kujua wamiliki halali na kusisitiza kuwa watendaji wa sekta ya ardhi lazima wafanye zoezi hilo kwa umakini na uaminifu mkubwa.


” Najua baada ya kutangaza zoezi hili la uhakiki baadhi ya Maafisa ardhi wataanza kuhangaika kuuza viwanja na wengine kunyofoa nyaraka, tumieni njia sahihi maana kila mtu ana haki ya kumiliki kiwanja zaidi ya kimoja cha msingi ni kufuata sheria.


Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi aliwapatia ankara za malipo ya ardhi wananchi 600 wa eneo la Kigoto kata ya Kirumba katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela lililokuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa eneo hilo na jeshi la Polisi.


” Ninyi wananchi wa Kigoto wamepatiwa eneo hili na Mhe. Rais John Pombe Magufuli bila kutozwa gharama za thamani ya ardhi na ndiyo ninyi pekee katika mkoa wa Mwanza mliopata eneo kwa gharama nafuu, mmuombee  Rais Magufuli kwa kuwapatia eneo” alisema Lukuvi.


Vile vile, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitangaza kuanza awamu ya pili ya mpango wa Funguka kwa Waziri utakaowezesha wananchi wenye migogoro ya ardhi  kujaza fomu maalum na kuiwasilisha ofisi za ardhi za mikoa kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi na Waziri.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ambaye ni Mbunge wa jimbo la Ilemela aliwahakikishia wananchi wa Ilemela kuwa serikali itahakikisha inamaliza migogoro yote ya ardhi katika mkoa wa Mwanza kama ilivyoshughulikiwa mgogoro wa Kigoto katika kata ya Kirumba mkoa wa Mwanza.


Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Eliah Kamyanda alisema mgogoro wa eneo hilo ulidumu kwa takriban miaka 30 mpaka mhe Rais aliporidhia wananchi hao kurejeshewa eneo hilo.


Alisema, mgogoro huo ulipitia hatua mbalimbali na kwa sasa kazi ya upimaji eneo hilo limekamilika na wananchi wapatao 600 wamepatiwa ankara za malipo ya kumilikishwa.



from MPEKUZI https://ift.tt/3ejbPPs
via IFTTT

No comments:

Post a Comment