Na Atley Kuni, Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo amewaagiza wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi Halmashauri, kuhakikisha shilingi bilioni 245.3 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo zinatumika kwa wakati kwenye miradi iliyokusudiwa na kwamba hatarajii kuona fedha hizo zinarudishwa hazina ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha.
Akizungumza na waandishi wa Habari, katika Makao Makuu ya Ofisi za TAMISEMI mjini Dodoma , Waziri Jafo amesema kuwa, ifikapo tarehe 30 Mei, 2021, kila halmashauri ihakikishe kuwa fedha zote zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maendeleo kama ujenzi wa madarasa, zahanati au majengo ya ofisi za serikali zinatumika ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa na thamani ya fedha ionekane.
Amesema kamwe, hatarajii kuona halmashauri yoyote iliyopokea fedha toka hazina, inapofika mwezi wa sita, ikishindwa kutumia fedha yote iliyopokea kwa visingizio vya aina yoyote ndiyo maana anawajulisha viongozi wakuu wa mikoa na kufuatilia mapema ili fedha zote zitumike kwa wakati muafaka kukamilisha miradi ya maendeleo iliyokusudiwa.
“Kwa hiyo niwatake wakuu wa Mikoa, wasimamie fedha hizi katika halmashauri zao, ninafahamu yawezekana wakuu wa Mikoa wengine saa hizi hawana taarifa kwamba kuna fedha zimeingia katika maeneo yao ya utawala, hususan ni katika halmashauri, ndio maana ninataka wakuu wa mikoa wakasimamie, kwanza kujua ni kiasi gani zimefika kwa kila halmashauri na pili kuhakikisha fedha zilizo ingia katika robo ya pili nay a tatu ya mwaka zinatumika ipasavyo na thamani ya miradi ionekane ifikapo Juni 30,2021” amesema Mhe. Jafo.
Waziri Jafo amesema kufikia sasa kiasi cha sh. bilioni 245 sawa na asilimia 38.9 ya fedha zote zilizotengwa na serikali cha Shilingi bilioni 629.1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 kimekwishatolewa, hivyo ni jukumu la wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi halmashauri kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika ipasavyo.
Amefafanua kuwa kiasi cha fedha kilichotolewa, kimeelekezwa katika miradi ya ujenzi wa majengo ya Utawala ya halmashauri, ujenzi wa wodi tatu katika hospitali 67 zinazoendelea kujengwa, ununuzi wa vifaa tiba, ujenzi wa Hospitali 27, ukamilishaji wa zahanati tatu kwa kila halmashauri, miradi ya elimu ikiwemo na ukamilishaji wa majengo ya madarasa.
Amesema katika mwaka wa fedha ulioisha wa 2019/20 fedha nyingi zilirudi hazina huku miradi mingi ikiwa haijakamilika, kwa hiyo amesisitiza kuwa hataki suala hili lijirudie tena mwaka huu.
Waziri Jafo, amesema yeye pamoja na Naibu Mawaziri wawili katika Ofisi yake muda wote watakuwa macho kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa kazi zinazo endelea.
from MPEKUZI https://ift.tt/2NTpx0S
via IFTTT
No comments:
Post a Comment